WAKATI Watanzania wakiendelea kuomboleza vifo vya wanajeshi saba wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), waliokufa katika Jimbo la Darfur nchini Sudani, askari wengine watatu wa jeshi hilo wamedaiwa kupoteza maisha.
Idadi hiyo imedaiwa kuongezeka, baada ya wanajeshi hao watatu ambao ni kati ya 14 waliokuwa wamejeruhiwa vibaya, nao kupoteza maisha katika shambulizi la kushtukiza.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya JWTZ, kimesema kuwa askari hao wamefariki dunia baada ya jitihada za madaktari kuokoa maisha yao kushindikana.
Askari hao walifariki baada ya kushambuliwa na kikundi cha waasi wa Sudani, walipokuwa katika msafara wa kusindikiza waangalizi wa amani kutoka Khor Abeche kwenda Nyara, katika Jimbo la Darfur.
MTANZANIA ilipomtafuta msemaji wa jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe kuzungumzia taarifa hizo, alisema hakuna taarifa zozote zinazoonesha kuwapo na ongezeko la idadi ya vifo vya Darfur, Sudani.
Kuhusu usafirishwaji wa miili ya askari hao kuja nchini, Kanali Mgawe alisema suala hilo la usafirishwaji wa miili ya askari hao, linaratibiwa na Umoja wa Mataifa (UN), ingawa JWTZ inafuatilia kwa karibu.
“Ninapenda kukuambia kuwa hadi sasa hakuna mwanajeshi aliyeongezeka, ila hizo ni taarifa ambazo si sahihi na zimekuwa zikienezwa katika mitandao ya kijamii. Sisi kama jeshi hatuna taarifa kama hizo,” alisema Kanali Mgawe.
Alipoulizwa kuhusu kutajwa kwa majina ya marehemu waliokufa katika tukio hilo la kushtukiza, Kanali Mgawe alisema jeshi haliwezi kutaja majina hayo kwa sasa, ila kinachofanyika ni kuwasiliana na ndugu wa marehemu hao.
“Safari hii asilimia kubwa ya askari wetu waliokwenda Sudan, wametoka katika mikoa ya mipakani, kwa hiyo tunachokifanya sasa tumeshawasiliana na makamanda wa kambi zote za jeshi ambazo wametoka marehemu hawa, ili waweze kuwasiliana na ndugu wa marehemu.
“Hivi ndugu utajisikiaje unasoma gazeti au unaangalia TV na kusikiliza redio halafu ukasikia kuwa ndugu yako amefariki utajisikiaje, ni lazima katika hili tuweze kufuata taratibu nzuri zinazokubalika kwa kuwasiliana nao moja kwa moja.
“Ninachotaka kuwahakikishia Watanzania kuwa JWTZ lipo imara na kama kuna taarifa yoyote tutaitoa mbele ya umma,” alisema.
Hata hivyo Kanali Mgawe alisema jeshi hilo limetuma ujumbe maalumu kwenda Darfur kuchunguza kiini cha tukio hilo, ingawa hakuweza kueleza kikosi hicho kinaundwa na wataalamu wa fani gani.
Source: Mtanzania