Polisi wa kimataifa Interpol, wamemuweka mwanamke aliyeshukiwa kuongoza mashabulizi ya kigaidi nchini Kenya raia Muingereza Samantha Lewthwaite, kwenye orodha ya watu wanaosakwa sana duniani.
Hatua hii ni kutokana na ombi la serikali ya Kenya kwa Interpol.
Bi Lewthwaite, mwenye umri wa miaka 29, ni mjane wa mlipuaji aliyefanya shambulizi la kujitoa mhanga mjini London Uingereza mwezi Julai mwaka 2005
Anajulikana kama "white widow", na amehusishwa na kundi la kigaidi la Al Shabaab nchini Somalia.
Polisi wa Interpol hata hivyo hawakuhusisha hatua ya kumsaka Samantha na shambulizi la kigaidi dhidi ya jumba la maduka la Westgate mjini Nairobi lililowaua watu 67.
Hata hivyo, hatua hii ya kumsaka Bi Lewthwaite inakuja punde baada ya shambulizi hili la kigaidi nchini Kenya.
Al-Shabab ilikiri kufanya mashambulizi hayo yaliyotokana na kutekwa kwa jengo la Westgate na kisha kutekwa kwa raia wa kawaida waliokuwa ndani ya jengo hilo kwa siku nne.
Kwa mujibu wa polisi wa Interpol, mwanamke huyo anasakwa na serikali ya Kenya kwa kumiliki mabomu na kupanga njama ya kufanya mashambulizi kuanzia Disemba mwaka 2011.
Ikiwa mwanamke huyo atakamatwa katika nchi mwanachama wa Interpol, atazuiliwa na kusibiri kupelekwa katika nchi anayotakikana kwa kesi kufunguliwa dhidi yake.
Bi Lewthwaite anajulikana kwa jina bandia la, "Natalie Webb" –na alikuwa anasakwa kwa madai ya kumiliki hati bandia ya usafiri nchini Afrika Kusini.
Ni mjane wa Germaine Lindsay, mmoja wa washambuliaji wanne waliohusika na shambulizi la kigaidi mjini London ambapo watu 52 waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa