Ni miaka 42 imefika tangu Shule ya Msingi ya Kibarashi iliyopo wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga kujengwa mwaka 1971 ikiwa haina vyoo vya kudumu hivyo uongozi wa shule wa wakati huo walilazimika kuchimba vyoo vya muda ili wanafunzi na walimu waweze kutumia.
Mkuu wa Shule ya Msingi hiyo, Fatuma Mahimbo anasema tokea mwaka 1971 shule hiyo ilipojengwa walimu na wanafunzi wanaendelea kutumia vyoo vya muda ambavyo ni hatari kwa usalama wa maisha yao.
Mahimbo anasema ameripoti shuleni hapo mwaka 2010 na kuikuta hali ya huduma ya vyoo ni mbaya, ambapo mwaka 2011 alijaribu kuomba fedha ya ujenzi wa vyoo hivyo kwenye Halmashauri ya Kilindi na kuelezwa kuwa mwaka huo wa fedha haijapangiwa kwenye bajeti.
““Mwaka 1971 shule hii ilijengwa bila ya kujengwa vyoo vya kudumu hivyo mimi hali hiyo nimeikuta nilikuja mwaka 2012 nimekikuta choo kilichopo hakifai kutumika hivyo tulilazimika kujenga choo cha nyasi kiweze kutumiwa na wanafunzi, huku walimu wakitumia choo kilichopo nyumbani kwangu ambayo ni nyumba ya walimu,”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema walikaa kikao cha kamati ya shule hiyo na kukubaliana suala hilo lipelekwe kwenye Serikali ya kijiji ili iweze kuwasaidia.
Anaeleza baada ya kuwasilisha suala hilo kwenye Serikali ya kijiji iliamua kujenga vyoo viwili kila kimoja kina matundu matano. Hivyo ujenzi huo umeishia kwenye linta kutokana na Serikali ya kijiji hicho kuishiwa fedha.
“Ujenzi huu umesimama mwaka 2012 hivyo tumekaa kikao na wazazi na tumekubaliana kila mzazi atachangia Sh2000 kuanzia Julai mwaka huu”anasema Mahimbo.
Mahimbo anasema kutokana na hali hiyo aliyaomba mashirika na taasisi mbalimbali yajitokeze yaweze kusaidia ujenzi wa vyoo vya shule ili kuokoa afya za wanafunzi ambazo zipo hatarini na hata jamii inayowazunguka kupata magonjwa ya milipuko.
Anasema jamii haina mwamko wa elimu hawatambui suala la kuchangia ujenzi wa choo linawahusu wao wanadhani suala hilo ni la mwalimu mkuu hivyo wanatakiwa kuchangia fedha ili ujenzi wa vyoo hivyo ukamilike