Makala-TIBA KWA VYAKULA

Imeandikwa na Sheikh Tariq Abdulaziz Mohamed


Orodha ya vyakula vifuatavyo vimeelezwa kuwa
na uwezo mkubwa wa kuimarisha kinga ya mwili
na kupambana na maambukizi mengine kwa
kuwa na kiasi kikubwa cha protini na virutubisho
vingine.
SUPU YA KUKU
Supu ya kuku wa kienyeji inaelezwa kuwa na
virutubisho vinavyosaidia kupunguza utokaji wa
makamasi. Utapata virutubisho vingi zaidi
ukitengeneza supu ya kuku kwa kuchanganya na
mboga za majani. Weka chumvi kiasi kidogo
katika supu hiyo.
VITUNGUU SAUMU
Vitunguu saumu vina kirutubisho aina ya ‘allicin’
ambacho kina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya
magonjwa mbalimbali ya kuambukiza. Kitunguu
saumu kinatoa kinga halikadhalika kinapunguza
muda wa mtu kuumwa na mafua. Tumia
kitunguu hicho kwa kupika kwenye chakula au
kwa kutafuna punje zake.
CHAI
Chai, hasa ya kijani, (green tea) ina virutubisho
vya kuimarisha kinga ya mwili. Utafiti wa hivi
karibuni uliofanywa na jarida moja la masuala ya
virutubisho nchini Marekani (Journal of the
American College of Nutrition) umeonesha kuwa
watu wanaotumia chai kwa mpangilio maalum
hawasumbuliwi mara kwa mara na mafua
pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza,
huwa salama na mafua au siku za kuumwa mafua
hupungua kwa asilimia 36 ukilinganisha na wale
wasiokuwa na kinga imara.
Hata hivyo, tahadhari inatolewa kwa watoto wa
shule kutokupewa kiasi kingi cha chai kwa siku.
Unywaji wa kikombe kimoja kwa siku kwa mtoto
wa shule siyo mbaya. Kwa mtu mzima, asizidishe
vikombe vitatu kwa siku. Ikumbukwe kuwa chai
inapotumika kwa wingi kupita kiasi, huweza
kusababisha pia tatizo la kukosa choo kwa muda
mrefu. Kunywa kiasi kwa afya yako.
MACHUNGWA, PILIPILI KALI
Utafiti unaonesha kwamba ulaji wa vyakula
vyenye Vitamin C kwa wingi kila siku husaidia
kuondoa au kuzuia ugonjwa wa mafua. Miongoni
mwa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha
Vitamin C ni pamoja na machungwa, mboga za
majani aina ya Brokoli na pilipili kali.
Ili kupata kiasi kingi cha Vitamin C, inashauriwa
machungwa yaliwe pamoja na nyama zake za
ndani au kunywa juisi yake.
ASALI
Kama inavyojulikana, asali ni tiba ya matatizo
mengi ya kiafya, miongoni mwa hayo ni pamoja
na mafua. Asali inasaida kuondoa kikohozi na
muwasho kwenye koo. Halikadhalika, asali
inaweza kutumiwa na watoto wadogo kama
dawa.
Watoto wanaoruhusiwa kutumia asali kama tiba
ni wa umri kati ya miaka 2 hadi 5. Hawa dozi
yao ni nusu kijiko kidogo cha asali, wenye umri
wa miaka 6-11 wapewe kijiko kimoja kidogo na
wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 18, wapewe
vijiko vidogo viwili vya asali wakati wa kulala.
MTINDI
Kutokana na kiwango kikubwa cha protini
ilichonacho, Mtindi ni chakula kingine
kinachofaa kuliwa na mtu mwenye mafua ili
kupunduza siku za kusumbuliwa na ugonjwa
kukohoa.
CHOKOLETI NYEUSI
Wataalamu wanakubaliana kuwa ulaji wa
‘chocolate’ nyeusi (dark chocolate) huimarisha
kinga ya mwili, hivyo inapoliwa na mgonjwa wa
mafua huweza kumpa ahueni mgonjwa kwa
namna moja ama nyingine. Halikadhalika huwa
kinga kwa maambukizi mengine.
PWEZA
Samaki aina ya pweza wana virutubisho vingi vya
kuongeza kinga ya mwili yenye uwezo wa
kupambana na bakteria pamoja na virusi vya
mafua. Kiasi kidogo cha pweza, awe wa
kukaangwa au kuchemshwa kama supu, anafaa
kuliwa mara kwa mara kuimarisha kinga ya
mwili.
VIAZI VITAMU
Kirutubisho aina ya ‘Beta-carotene’ huimarisha
kinga ya mwili. Kirutubisho hicho huwa ni
muhimu kwa ustawi na uimarishaji wa kinga
mwilini na kinapatikana kwa wingi kwenye viazi
vitamu na vyakula vingine kama vile karoti,
maboga na mayai, (kiini).
Kwa ujumla, suala la kuimarisha kinga ya mwili
ni muhimu kwa afya zetu. Ulaji wa vyakula
vilivyotajwa hapo juu na vingine, unatakiwa
kuwa ni wa mara kwa mara kama siyo wa
kudumu, kwa sababu mwili unapokosa kinga
imara, ni rahisi kushambuliwa na maradhi ya
kuambukiza kila mara
Share: