SHORT HISTORY-LANGA "DAWA ZA KULEVYA ZILINIPOTEZEA MALENGO"

Huyu ni mmoja wa matunda ya shindano la muziki la Coca-Cola Pop Stars mwaka 2004 ambalo washindi wake waliounda kundi la Wakilisha.

Mbali ya Langa, wengine ni Sarah Kaisi `Shaa’ na Witness Mwaijaga `Witness’. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa kung’ara kisanii kwa wakali hao, ingawa kwa sasa kundi hilo limesambaratika, kila mmoja akitamba kivyake.

Lakini kwa bahati mbaya, mmoja wao, Langa kwa miaka ya hivi karibuni hakusikika kabisa, jambo lililomlazimu mwandishi wa makala haya kumtafuta sababu za ukimya wake.

Haikuwa kazi rahisi, lakini hatimaye Langa alipatikana na bila kutafuna maneno alisema kwamba, alishindwa kufanya kazi baada ya kuwa `teja’ aliyekubuhu.

Yaani alizama katika matumizi ya dawa za kulevya kiasi cha kupoteza kabisa mwelekeo si wa kisanii pekee, bali hata kimaisha.

“Siyo siri, kilichokuwa kimenifikisha katika hali hiyo ni dawa za kulevya. Kwa miaka mitano nilitumia sana Cocaine, Heroin, bangi na pombe. Namshukuru Mungu sasa nimerejea katika hali yangu…

“Siamini kama nimenusurika kwa sababu madawa yalinitesa, nikafanya mengi ya ajabu yaliyoichukiza familia yangu na marafiki ikiwa pamoja na kuwa mwizi na mkabaji mitaani na nyakati za usiku,” anasema Langa ambaye kundi lao la Wakilisha lilitamba na nyimbo kama `Unaniacha Hoi’ na `Kiswanglish’.

Anaeleza kwamba, kwake hayo ndiyo aliyoyaona maisha yanayomfaa, akidai awali alikuwa amechoshwa kuishi kwa masharti kutoka kwa wazazi wake waliokuwa wanampa mwongozo wa maisha, lakini bila kujua akadhani `anachungwa’.

Kwamba, umaarufu na ngekewa ya kuzishika pesa katika umri mdogo kupitia muziki vilimtia kiburi zaidi, na hivyo kuamua kujitenga kabisa na familia yake iliyomlea kwa mapenzi mazito.

“Niliamini naweza kujitegemea kupitia kazi yangu ya muziki, nikajichanganya mtaani,” anasema kijana huyo aliyetoa kibao chake cha kwanza, Matawi ya Juu mara baada ya kusambaratika kwa kundi la Wakilisha kutokana na kila mmoja kuamua kujitegemea kimuziki. Na kweli, Matawi ya Juu ilidhihirisha kuwa Langa ni moto wa kuotea mbali katika fani. Aliweza kusimama kwa miguu yake na kutikisa.

Mwenyewe anasema: “Jina hilo la Matawi ya Juu lilidhihirisha hivyo pale video ya kibao hicho ilipotajwa kuwania Tuzo za MTV Base kwa upande wa hapa Bongo miaka michache iliyopita, kisha kutwaa Tuzo ya Kisima nchini Kenya. “Moto huo uliwafanya baadhi ya wasanii wakongwe katika gemu ya Bongo Fleva kunitafuta na kunipa majukumu ya kushiriki katika kazi zao, ikiwemo Chagua Moja ya Farid Kubanda `Fid Q’.

“Baada ya kuona wakongwe wamekubali vitu vyangu na kuanza kunishirikisha…nikapata pia safari za nje ya nchi. Huko Nairobi (Kenya) niliweza kufanya kazi na vichwa vikali vinavyounda Kundi la Necessary Noise, Naaziz na Wyre (Kevin Wyre)….”


Share: