ELIMU NI TATIZO KUBWA - MKAPA

RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amesema Watanzania wamejenga tabia ya kulalamika bila kutambua kwamba elimu ndiyo chanzo cha matatizo yote. Kauli hiyo aliitoa juzi, wakati wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Maktaba na Maabara la Chuo Kikuu cha Bugando, jijini Mwanza, ambako jumla ya Sh milioni 400 zilichangishwa. Kauli hiyo ya Mkapa inafanana na ile iliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.


Lowassa amekuwa akisisitiza juu ya umuhimu wa suala la elimu kupewa kipaumbele, akiamini kuwa kuboresha sekta hiyo ndio suluhu ya matatizo mengine yote yanayowakabili Watanzania, ukiwemo umaskini.

“Watanzania tumejenga tabia ya kulalama kwamba ingawa nchi ina rasilimali tele, pamoja na rasilimali watu, bado wananchi wana umasikini wa kutupa, lakini hatuna budi kutambua kwamba hata tungelikuwa na watu wengi namna gani, kama hawana elimu ni vigumu kujiwezesha kuendelea, na ni vigumu kushawishi walioendelea kuja kutusaidia kujiendeleza,” alisisitiza Mkapa juzi, wakati wa harambee hiyo.

Akimnukuu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mkapa alisema mara nyingi alikuwa akitumia usemi wake kuwa “Elimu ni ufunguo wa maisha, maisha bora ya watu na nchi endelevu bila elimu hakuna maendeleo yoyote”.

Mkapa alisema kuanzishwa kwa Chuo cha Kikuu cha Tiba Bugando (CUHAS) kwa ajili ya kufundisha madaktari na watumishi wengine wa afya wenye tunu zaidi, ni dhahiri CUHAS itaendeleza jitihada katika azma yake ya kutoa watumishi stadi na mahiri wenye kufuata maadili ya kazi katika sekta ya afya.

Aliupongeza uamuzi wa Baraza la Maskofu Katoliki nchini kwa kuthubutu na kuanzisha chuo hicho kwa kupambana na maadui ujinga, maradhi na umasikini.

Katika harambe hiyo, Mkapa alichangia Sh milioni 10, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Sh mil.10), wafanyakazi wa Hospitali ya Bugando Sh mil. 100.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Sh mil. 45, Chuo cha SAUT Sh mil. 10, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira Sh mil.8, MNEC wa Tarime Christopher Gachuma Sh mil. 5 na Benki ya CRDB Sh mil.3.

Wengine ni Meya wa Jiji la Mwanza, Stanislaus Mabula Sh mil. 1.5, Kampuni ya Nyanza Road Ltd Sh mil. 5, Naibu Waziri Charles Kitwanga ‘Mawe matatu’ mil.3, PPF Mkurugenzi Mkuu wake William Urio Sh mil. 11, CCM Mkoa wa Mwanza Sh mil.1, Mathias Manga Sh mil. 2.3, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja Sh mil. 10, Anthon Dialo (Sahara Group) Sh mil.7 na Familia ya Baba wa Taifa, ikiwakilishwa na mwanae Madaraka Nyerere, ng’ombe watatu.

Awali kabla ya kuanza kwa harambee hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Jackob Mtabaji, alisema CUHAS kwa sasa ni chuo kikuu kamili ambapo mwaka 2003 kilipoanzishwa kilijulikana kama Chuo kishiriki cha Mt. Agustino cha Tanzania (SAUT) na kwa muda mfupi kilipiga hatua na kupanda hadhi.

Profesa Mtabaji alisema kwamba jengo hilo litakapokamilika litajulikana kwa jina la Mwalimu Julius Nyerere Learning Resource Center, ambapo juhudi za kuanzishwa kwake zilitokana na uamuzi wa Baraza Kuu la Maskofu Katoliki Tanzania na uongozi wa Chuo Kikuu cha CUHAS kutambua umuhimu wa kuwa na jengo hilo litakalosaidia wanachuo kuwa na maarifa zaidi.


Share: