Makala Maalum-HISTORIA YA BARRACK OBAMA

Barack Hussein Obama II (amezaliwa 4 Agosti 1961) ni rais wa 44 na rais wa sasa wa Marekani.
Yeye ni Mwafrika-Mwamerika wa kwanza kushika wadhifa huo, na pia mtu wa kwanza mwenye kuzaliwa Hawaii kuwa rais wa Marekani.
Obama awali alihudumu kama Seneta mdogo kutoka jimbo la Illinois, tangu Januari 2005 hadi alipojiuzulu baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2008, mwezi wa Novemba.
Obama alifuzu mwanzo kutoka katika chuo kikuu cha Columbia University, kisha akafuzu katika masomo ya kisheria kutoka katika kitivo cha masomo ya sheria kwenye chuo kikuu cha Harvard, ambako alikuwa rais wa jarida la Harvard Law Review. Alihudumu baadaye kama mwana-harakati wa mambo ya kijamii, kabla ya kuhitimu katika masomo ya kisheria. Hatimaye, alifanya kazi kama wakili wa haki za umma mjini Chicago, kisha akafunza sheria ya kikatiba katika Chuo Kikuu cha Chicago kuanzia 1992 hadi 2004.
Obama alihudumu mihula mitatu katika Bunge la jimbo la Illinos (Illinois Senate) tangu 1997 hadi 2004. Baada ya kushindwa katika jitihada zake za kuchaguliwa katika Bunge Dogo la Marekani mwaka 2000, Obama alisimama kuchaguliwa katika Bunge La Maseneta La Marekani mwaka 2004. Alishinda uchaguzi hapo Novemba 2004.
Alitangaza kusimama kuchaguliwa kama rais wa Marekani mwezi Februari, mwaka 2007. Baada ya kampeni kali katika uteuzi wa chama cha Democratic Party dhidi ya Hillary Clinton, aliteuliwa kama muania-kiti cha urais kwenye tikiti ya chama hicho. Katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2008, alimshinda John McCain, aliyekuwa ameteuliwa na chama cha Republican Party, na akaapishwa kama rais tarehe 20 Januari 2009. Tarehe 9 Oktoba 2009, Obama alituzwa kwa Tuzo ya Nobel ya Amani.


UTOTO WAKE
Baba yake Obama alikuwa Mkenya Barack Obama aliyeaga dunia 1982. Mzee Obama alitoka mkoa wa Nyanza nchini Kenya akaenda Marekani masomoni. Mama yake, Ann Dunham, alikuwa Mwamerika mzungu kutoka jimbo la Kansas aliyeaga dunia 1995. Wazazi walifunga ndoa wakati ndoa kati ya watu weupe na weusi bado ilikuwa marufuku katika sehemu za kusini za Marekani. Wazazi waliachana baada ya miaka miwili na mtoto Barack alibaki na mama.
Baadaye mama yake aliolewa na mwanafunzi kutoka Indonesia akamfuata aliporudi kwake. Hivyo Barack aliishi Jakarta hadi 1971 aliporudi Marekani na kukaa na babu yake huko Hawaii hadi alipomaliza shule ya sekondari.
Barack ana dada mmoja kutoka ndoa ya pili ya mama yake na baba ya kabo kutoka Jakarta Indonesia


MASOMO NA KAZI YAKE
Baada ya kumaliza masomo ya sekondari alisomea masuala ya siasa na sheria katika vyuo vya Occidental huko Los Angeles, Columbia huko New York na baadaye chuo kikuu cha Harvard. 1991 alimaliza kwa shahada ya dokta.
Baada ya shahada ya kwanza Obama aliwahi kufanya kazi ya kijamii huko Chicago. 1991 alirudi Chicago alipopata kazi katika ofisi ya wanasheria akafundisha pia kozi za sheria kwenye chuo kikuu cha Chicago


SIASA
1996 alichaguliwa kama seneta wa bunge la Illinois akarudishwa 1998 na 2002. 2004 alichaguliwa kuwa seneta wa bunge la kitaifa.
Mwezi wa Februari 2007 alitangaza ya kwamba atatafuta nafasi ya mgombea wa urais upande wa chama cha kidemokrasia. Katika kampeni ya kitaifa ndani ya chama chake alifaulu kumshinda mgombea mwenzake mama Hillary Clinton. 28 Agosti 2008 aliteuliwa na mkutano wa chama cha kidemokrasia kuwa mgombea wa chama hicho kwa uraisi. Katika uchaguzi wa Novemba 2008 alimshinda mgombea wa chama cha kijamhuri seneta John McCain

FAMILIA YAKE
Obama alimwoa Michelle Robinson ambaye ni mwanasheria kama yeye mwenyewe. Wana mabinti wawili Malia Ann (*1998) na Natasha (*2001) anayeitwa Sasha. Familia ina nyumba yake huko Chicago


TUZO YA NOBEL YA AMANI

Mwaka wa 2009 aliteuliwa kwa Tuzo ya Nobeli ya Amani "kwa jitihada zake za kuimarisha diplomasia ya kimataifa na ushirikiano kati ya mataifa"



Share: