Dar es Salaam
. Maelfu ya wakazi wa D Dar es Salaam, walijitokeza kwa wingi jana kumlaki Rais wa Marekani, Barack Obama aliyewasili nchini kwa ziara ya siku mbili inayohitimishwa leo huku wakilalamikia kutomwona.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, msafara wake ulipitia Barabara za Nyerere, Nkrumah, Samora, Magogoni hadi Ikulu.
Ukonga Majumba Sita
Wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto, Ukonga, Kitunda, na Tabata walifurika eneo la Majumba Sita kwa ajili ya kumwona, lakini hali ilikuwa tofauti.
Magari yalizuiwa kuanzia Njia panda ya Segerea na hayakuruhusiwa kusogea karibu na barabara inayotoka uwanja wa ndege. “Mimi nimefika hapa kwa ajili ya kumwona, sikumwona jamani yaani nimepigwa na jua bure,” alilalamika dada mmoja akiwa na wenzake huku ameshikilia kandambili mkononi.
Naye Mkazi wa Tabata Mawezi, aliyejitambulisha kwa jina la Jana Kamanzi alilalamikia mwendo kasi wa magari hayo na kushindwa kumuona kiongozi huyo.
Kipawa/Jeti Lumo
Maeneo hayo walijitokeza watu wengi huku wengine wakiwa na mikeka ya kukalia tayari kumlaki kiongozi huyo.
Gazeti hili lilishuhudia umati huo kwa wakazi kutoka maeneo ya Jeti, Kipawa, Karakata waliofika kumlaki Rais huyo wa Marekani.
Baadhi ya mama lishe walitumia nafasi hiyo kuuza chakula kwenye ndoo za plastiki kwa kificho, huku wafanyabiashara ya maji na wao wakitumia nafasi hiyo kupandisha bei ya maji huku wakiuza kwa kificho.
Vingunguti
Katika maeneo ya Vingunguti, umati ulifurika pande zote mbili za barabara kwa wakazi wa Vingunguti na Kijiwe Samli wakiwamo wafanyakazi ambao ofisi zao ziko karibu na Barabara ya Nyerere.
Source Mwananchi