WALIMU WACHAPWA BAKORA NA WAZAZI

Kundi la wazazi wa watoto wanaosoma katika Shule ya Msingi Kinole, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro, wamevamia shule hiyo na kuwachapa walimu bakora na kusababisha baadhi yao (walimu) kujeruhiwa.
Habari kutoka shuleni hapo zilizothibitishwa na Ofisa Elimu wa Halmashauri hiyo, Donald Temba, zinaeleza kuwa wazazi hao walifanya kitendo hicho juzi wakidai kuchoshwa na vitendo vya walimu hao vya kuwachapa watoto wao.
Kutokana na tukio hilo, uongozi wa halmashauri umeifunga shule hiyo hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa.
Akielezea tukio hilo, Temba alisema lilifanywa na wazazi hao baada ya walimu kutoa adhabu kwa wanafunzi kwa makosa waliyofanya.
Alisema wazazi hao walivamia shule hiyo wakimtuhumu Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Jaka Lukome, kuwachapa wanafunzi wawili bakora.
Kwa mujibu wa Temba, wanafunzi hao walichapwa bakora siku mbili zilizopita kutokana na kosa la kupigana wakiwa shuleni.
“Kuna adhabu zilikuwa zimetolewa kwa wanafunzi wawili wa shule hiyo. Ndiyo kikawa chanzo cha wazazi hao kuandamana na kuvamia shuleni hapo na kuwapiga bakora walimu,” alisema Temba.
Hata hivyo, alilaani kitendo cha wazazi kuvamia shule na kuwachapa walimu bakora.
Alisema kitendo hicho kinaweza kuzorotesha maendeleo ya elimu katika kijiji cha Kinole kutokana na walimu kuogopa kufanya kazi katika shule hiyo.
Aliutaka uongozi wa serikali ya wilaya ya Morogoro kuwachukulia hatua za kisheria wazazi waliofanya kitendo hicho kwa kuwa kimewadhalilisha walimu mbele ya wanafunzi wa shule hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Julius Madega, alisema wamefikia hatua ya kuifunga shule hiyo baada ya kutokea vurugu hizo na hivyo kuhatarisha amani dhidi ya wazazi na walimu.
Alisema wanakusudia kuwahamisha baadhi ya walimu na kuwapeleka shule nyingine, akiwamo mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Nao wakazi wa wilaya hiyo, Gladness Masimba na Abdallah Mwombosa, walilaani kitendo cha wazazi hao kuwachapa walimu bakora.
Walisema kitendo hicho ni kibaya kwani kitachangia kuua elimu katika kijiji hicho.
Waliutaka uongozi wa wilaya kuwachukulia hatua kali wazazi hao ili kukomesha tabia hiyo kwa wengine wanaofikiria kufanya kitendo hicho.
Hata hivyo, kufuatia vurugu hizo Jeshi la Polisi Wilaya hiyo ya Morogoro inawashikilia wahusika wa tukio hilo na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani

PICHA HII SIO YA SEHEMU LA TUKIO NI MFANO


Popular posts from this blog