Simba imeweza kuwabana mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa kusawazisha magoli waliyofungwa na kumaliza mchezo wakiwa na sare ya 3-3 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Sare hiyo imezidi kuwafanya mashabiki wa soka waelewe siku zote kwamba mpira ni dakika 90 au mpaka pale filimbi ya mwisho itakapopulizwa na mwamuzi wa kati aliyepewa dhamana ya kuchezesha mechi.
Alikuwa ni Mrisho Ngassa, ambaye alirejea Yanga msimu huu kwa kuanza kuifungia timu yake goli la kwanza katika dakika ya 14 akimalizia pasi fupi ya Hamisi Kiiza ambapo na shuti lake lilisindikizwa wavuni na beki wa Simba, Joseph Owino aliyekuwa kwenye jitihada za kuokoa shambulio hilo bila mafanikio.
Mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki zaidi ya 40,000 ilionekana kwamba ni neema kwa Wana-Jangwani pale walipofanikiwa kufunga goli la pili kupitia kwa Mganda Kiiza aliyemalizia mpira uliorushwa na Mbuyu Twite.
Yanga iliendelea kuwanyanyasa watani zao pale walipofunga goli la tatu kupitia kwa aliyeunganisha pasi ya Didier Kavumbagu na kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa magoli 3-0 na mashabiki wao wakiamini siku ya kulipiza kisasi cha 5-0 walichokipata Mei 6 mwaka jana kitatimia.
Hali ilikuwa tofauti kilipoanza kipindi cha pili baada ya King Kibaden, kocha mkuu wa Simba kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kuwaondoa Abdulhalim Homuod na Haroun Chanongo na nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na William Lucian ‘Gallas’.
Simba ilianza kucheza kwa kuelewana na safu ya kiungo ambayo ilikufa katika dakika 45 za kwanza ilifufuka na kuanza mashambulizi kuelekea kwenye lango la wapinzani wao.
Betram Mombeki alifanikiwa kuwasimamisha mashabiki wa Simba katika dakika ya 54 kwa kufunga goli la kwanza huko Owino akifunga goli la pili kwa kichwa dakika tatu baadaye na kuwanyamazisha Wana-Yanga ambao hawakuamini kilichokuwa kinaendelea kwenye mchezo huo.
Dakika ya 83, beki mpya wa Simba kutoka Burundi, Gilbert Kaze, aliunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na nahodha wake, Nassor Masoud ‘Chollo’ na kuisawazishia timu yake goli la tatu.
Yanga ilionekana kuridhika na matokeo ya kuongoza 3-0 na kuwafanya wachezaji wake wacheze na jukwaa katika kipindi cha pili.
Pia kila mmoja alionekana anataka kufunga na kushindwa kucheza kiufundi kama walivyofanya katika dakika 30 za kwanza za mchezo hali ambayo iliwagharimu na hawataweza kuisahau kwenye kumbukumbu zao.
Simba baada ya kuonekana kuzidiwa mchezo, iliingia kipindi cha pili ikiwa makini kwa kulinda lango lao na vile vile ikifanya mashambulizi kwa kutumia pasi fupi fupi.
Mabadiliko yaliyofanywa yalionekana kuzaa matunda kwa kutengeneza nafasi tano za wazi na tatu kati ya hizo zilizaa magoli.
Kutokana na matokeo hayo bado Azam iliyocheza mechi 10 inaendelea kuongoza ligi sawa na Mbeya City kila mmoja akiwa na pointi 20 na Simba iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 19.
Simba na Yanga yenye pointi 16 iliyo katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi zenyewe zimecheza mechi tisa.
Simba- Abel Dhaira, Nassor Masoud, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhan Singano ‘Messi’, Abdulhalim Homoud/ Said Ndembla, Betram Mombeki/ Zahor Pazi, Amissi Tambwe na Haruon Chanongo/ William Lucian.
Yanga- Ally Mustapha ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza/ Simon Msuva.