TAMKO LA SERIKALI POLISI KUUWA RAIA

Dar es Salaam.
 Serikali imetoa tamko bungeni kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi ikieleza kuwa sheria ya kanuni ya adhabu inaruhusu kutumia nguvu za kadiri hata kiasi cha kusababisha madhara au kifo.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kunukuliwa bungeni akiwataka polisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu wote wanaokaidi kutii sheria.

“…Nasema wapigwe tu, maana tumechoka sasa,” alisema Pinda alipojibu maswali ya papo hapo Alhamisi iliyopita.

Akisoma tamko hilo bungeni jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema kuwa kifungu cha 18(B) na 18(C) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatoa uwezo kisheria wa kutumia nguvu za kadiri hata ikibidi kiasi cha kusababisha madhara au kifo katika mazingira ya kisheria.

Aliyataja mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuokoa uhai wa mtu mwingine, kuzuia madhara makubwa ya mwili yasitokee kwake au kwa mtu mwingine na kumzuia mtu anayetenda tendo ovu la kubaka au kunajisi mtoto au kufanya vitendo kinyume na maumbile.

Pia kumzuia mtu anayevunja nyumba usiku au unyang’anyi wa kutumia silaha au kuchoma nyumba moto au kufanya kitendo chochote kinachohatarisha uhai wa mtu au mali.

Alieleza kuwa Kifungu cha 18 na 18(A) cha Sheria ya Adhabu Sura namba16 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002, kinampa haki mtu yeyote akiwemo askari kujilinda, kumlinda mtu mwingine, kulinda mali yake au mali ya mtu mwingine ikiwemo ya Serikali na taasisi zake, ambayo iko chini ya uangalizi wake kisheria.

Kauli hiyo ya Serikali kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi, ilitolewa ikiwa ni ufafanuzi wa jibu la swali la nyongeza lililoulizwa bungeni Mei 28,2013 na Rashir Ally Abdalah (Tumbe-CUF), ambapo Silima alisema mauaji yanayofanywa na askari polisi ni mauaji ya kisheria. Kutokana na kauli hiyo, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashi Mohammed aliomba mwongozo wa spika kupata ufafanuzi wa kauli hiyo, na jana Silima kutoa kauli ya Serikali kujibu mwongozo huo.

“Ikumbukwe pia kuwa, kifungu cha 29 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi Sura322, pamoja na Kanuni za Kudumu za Utendaji za Jeshi la Polisi Na274, vinampa haki ya kisheria askari polisi kubeba na kutumia silaha za moto ikiwamo bunduki na mabomu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku..,”alisema Silima.

Alifafanua kwamba katika kutafsiri sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ikiwamo alizozitaja, mahakama katika nyakati tofauti imetoa msimamo wa kisheria juu ya suala hilo.

Akitoa mfano alisema: “Mathalan katika kesi ya Seif Mohamed Senzagala dhidi ya Jamhuri ya mwaka 1994 kama ilivyonukuliwa na Tanzania Law Report ukurasa wa 122, ambapo mshitakiwa (mwomba rufaa) alimjeruhi kwa panga mlalamikaji ambaye alimfuata nyumbani kwake na kuanza kumshambulia.”

Alisema katika kesi hiyo,mahakama ya rufaa pamoja na kuridhia uamuzi wa mahakama ya awali wa kumtia hatiani kwa kutumia nguvu kupita kiasi, ilibainisha kuwa mshtakiwa hakustahili adhabu kwani alitenda kosa lile wakati akijihami dhidi ya mashambulizi toka kwa mlalamikaji

source mwananchi.

Popular posts from this blog