MAJAMBAZI YATEKA GARI NA KUPORA SIMU,FEDHA NA BUNDUKI

Majambazi yateka mabasi, yampora polisi bunduki
Majambazi 10 wakiwa na silaha za kivita, wameteka mabasi mawili ya abiria katika Hifadhi ya Taifa Biharamulo na Burigi mkoani Kagera na kupora bunduki moja ya polisi waliokuwa wakisindikiza moja ya mabasi hayo pamoja na kuwapora abiria mali za aina mbalimbali.
Kufuatia tukio, Jeshi la Polisi Mkoani Kagera kwa kushirikiana na vikosi vingine vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeanza msako mkali katika hifadhi hizo kwa lengo la kuwakamata majambazi hao.
Mabasi hayo ya kampuni ya NBS lenye namba za usajili T 644 BUK likitoka Bukoba kwenda Arusha na kampuni ya RS Investment lenye namba za usajili T 495 AGT likitoka Bukoba kwenda Dar es Salaam, yalitekwa juzi saa 2:30 asubuhi.
Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Philip Kalangi, alifafanua kuwa majambazi hao walikuwa na bunduki mbili za Light Machine Gun (LMG) na sita aina ya Sub Machine Gun (SMG).
Kamanda Kilangi alisema majambazi hayo yalipora bunduki moja ya Jeshi la Polisi yenye namba za usajili 14302551 ambayo ilikuwa na askari wanne walikokuwa ndani ya gari wakilisindikiza moja ya mabasi hayo.
Hata hivyo, alisema askari hao walizidiwa nguvu na majambazi hao waliokuwa na silaha za kivita.
Alisema wakati wa majibizano ya risasi kati ya polisi na majambazi, abiria Frederick Rugahyula (47), alijeruhiwa shingoni na amelazwa katika Hospitali Teule ya Biharamulo akipatiwa matibabu.

Habari imetolewa na NIPASHE
Share: