MSAFARA WA OBAMA WAVAMIWA NA WANANCHI

Baadhi ya wakazi hao walisikika wakilalamika kutomwona Rais Obama kwani walitarajia angekuwa kwenye gari la wazi waweze kumuona.

Wakazi wengine walilalamikia hali hiyo, mbali na kutotarajia umati na kushindwa kumwona, walijua kuwa atakuwa kwenye gari la wazi ambalo wangeweza kumuona.

Makutano ya Mandela na Nyerere (Tazara)

Wananchi walivamia msafara wa Rais Obama katika eneo la Tazara na kusababisha msafara huo kupunguza mwendo.

Kitendo hicho kilitokea wakati Rais huyo na msafara wake uliokuwa na zaidi ya magari 15 ukitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ukienda Ikulu.

Msafara wa Rais Obama haukuwa katika mwendo wa kasi na ulipokaribia makutano ya barabara hizo maeneo ya Tazara, wananchi walivuka kutoka upande wa pili kushuhudia msafara huo kwa ukaribu zaidi.

Kitendo hicho cha wananchi kuvamia msafara huo kwa ghafla kiliwachanganya askari polisi waliokuwa wachache, hivyo kusababisha msafara huo kupunguza mwendo.

Awali askari Polisi waliimarisha ulinzi na kuwazuia watu kuvuka barabara kutokana na magari kupita kwa kasi eneo hilo na wananchi walitiii amari hiyo.

Njia Panda ya Veta

Katika maeneo yanayounganisha Barabara ya Nyerere na Chang’ombe, polisi walifanya kazi ya ziada kuzuia mamia ya watu waliofika kumlaki .

Mamia ya watu hao kutoka Temeke, Chang’ombe, Tandika, Ilala walifurika katika eneo hilo kutaka kumuona kiongozi huyo, lakini hata hivyo wengi walisikika pia wakilalamikia kutomwona.

Kamata

Wakazi wa maeneo ya Kariakoo, Gerezani, Ilala walifurika kuanzia njia panda ya Shauri Moyo huku wakiwa katika hali ya utulivu.

Polisi walikuwa na kazi ya kuzuia wakazi hao waliokuwa wanavuka barabara kabla na baada ya misafara kupita.

Mtaa wa Nkrumah

Hali ilikuwa tete katika Mtaa wa Nkrumah ambako ulipita msafara wa Obama wakati akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.Msafara wa Rais Obama ulipita katika Mtaa wa Nkrumah kwa ajili ya kuingia Mtaa wa Samora kuelekea Ikulu.

Maduka na ofisi kadhaa zilizoko maeneo ya Nkrumah, Kidongo Chekundu na Mnazi Mmoja yalifungwa kutokana na watu kuwa na hamu ya kuuona msafara wa Obama. Watu walikuwa wengi pande zote za barabara na msafara wa Obama ulipofika kwenye eneo hilo, watu walimshangilia kwa nguvu.

Hata hivyo, watu wengi walisikitishwa na kitendo cha kutomwona Obama kwani wengi walitegemea kuwa watapanda gari lenye vioo ambavyo wangeweza kumwona kwa urahisi wakati akipita katika eneo hilo la Nkrumah.


Source Mwananchi
Share: