PILIKA ZA UCHAGUZI ZIMBABWE

Vyama viwili vya kisiasa nchini Zimbabwe vimemuunga mkono waziri mkuu Morgan Tsvangirai katika uchaguzi  ujao wa urais.Vyama hivyo vimeahidi kuunda serikali ya umoja baada ya uchaguzi ulopangwa kufanyika Julai 31.

Jumatatu waziri wa fedha wa zamani ambaye pia hapo zamani alikuwa mshirika wa karibu wa  rais Robert Mugabe, Simba Makoni alisema kuwa ameunda ‘chama mseto cha mabadiliko’ na waziri mkuu Morgan Tsvangirai  pamoja na chama kingine cha kisiasa  kwa  lengo la kumshinda bw. Mugabe katika uchaguzi wa Julai 31.

Uamuzi huo wa kuunda ushirika wa vyama huenda ulitokana na somo waliojifunza kufuatia uchaguzi wa  urais wa mwaka elfu 2008 ambapo bw. Tsvangirai alishindwa kupata wingi wa kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi.Katika uchaguzi huo bw. Makoni alipata asili mia 9 za kura.

Katika ufunguzi wa kampeni zake Jumatatu bw. Tsvangirai alisema atagombania urais Julai 31, licha ya ukosefu wa mabadiliko ya kidemokrasia katika taifa hilo.

Kwa sasa uchaguzi nchini Zimbabwe unategemewa kuendelea lakini wizara ya fedha haina  takriban dola millioni 132 zinazokadiriwa kuhitajika kufadhili uchaguzi huo.
Waziri wa fedha wa zimbabwe Tendai Biti anasema bw. Mugabe lazima asukume makampuni ya migodi ya almasi kutoa  fedha za mauzo ya madini iwapo taifa hilo litaweza kupata fedha za kufadhili uchaguzi huo.


Share: