Gari limelipuka ndani ya soko rasmi mjini Mogadishu nchini Somalia.
Kwa mujibu wa polisi, hakuna taarifa zaidi kuhusu waliojeruhiwa katika shambulizi hilo kwenye soko la Bakara.
Somalia
Walioshuhudia shambulizi wanasema kuwa gari lilikuwa limewabeba watu waliokuwa wamevelia magwanda ya jeshi.
Hakuna kundi lolote limekiri kufanya shambulizi hilo, lakini kundi la wapiganaji wa kiisilamu wa al-Shabab, limekuwa likifanya mashambulizi ya kuvizia tangu kuondolewa kutoka mjini Mogadishu mwaka 2011.
Polisi walifahamisha BBC kuwa afisaa mkuu wa polisi amejeruhiwa kwenye shambulizi hilo, lakini hakuna taarifa zaidi hadi uchunguzi utakapokamilika.
Afisaa wa polisi Mohamed Hussein, alisema bomu lilikuwa limefichwa ndani ya gari la kijeshi, na limewajeruhi wanajeshi watano wa serikali.
Naye Hussein Nur, ambaye ni mfanyabiashara wa pesa, alisema alishuhudia gari likilipuka.
Kundi la Al-Shabab linapigana likitaka kuruhusiwa utawala wa kiisilamu nchini Somalia na licha ya kufurushwa kutoka mji mkuu Mogadishu katika miaka miwili iliyopita,lingali linadhibiti sehemu kubwa ya nchi.
Wanajeshi 18,000 wa Afrika, wako nchini Somalia kuunga mkono serikali ya Somalia iliyo chini ya rais Hassan Sheikh Mohamud, aliyechaguliwa na wabunge mwaka jana