Kiongozi wa zamani wa waasi ambaye alifanya mapinduzi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati Michel Djotodia ameapishwa kama rais.
Bwana Djotodia ameahidi kuandaa uchaguzi kufikia mwanzo wa mwaka ujao. Tangu achukue uongozi mwezi Machi kupitia kikundi cha waasi wa Seleka nchi hiyo imetajwa kutumbukia zaidi katika umaskini na utovu wa sheria.
Shirika la Umoja wa mataifa linakadiria kuwa zaidi ya thuluthi moja ya raia wa nchi hiyo wanahitaji msaada wa dharura.
Baraza la uslama la Umoja wa mataifa limeonya kuwa kuongezeka kwa ukatili na uvunjifu wa sheria katika Jamhuri ya Afrika ya Kati inatishia usalama na uthabiti wa eneo lote.
Msemaji wa rais wa zamani Francois Bozize ambaye aling'olewa madarakani na bwana Djotodia amemtaja kiongozi huyo mpya kama 'kibaraka'.
Msemaji huyo Levi Yakete, amenukuliwa katika Redio Ufaransa kusema:
'Bwana Djotodia, ambaye ameingia madarakani kwa njia ambazo sote tunaelewa, ni kibaraka tu wa Chad na Sudan. Aliingia madarakani kupitia njia ambazo hazikubaliki na watu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Alipindua utawala wa kisheria na katiba, ambao ulikuwa unaongozwa na Francois Bozize.'
Michel Djotodia rais wa CAR