WAHAMIAJI HARAMU KURUDISHWA KWAO

Serikali ya Tanzania  imefafanua zoezi la Serikali hiyo la kutaka kuwaondoa wahamiaji haramu walioko katika mikoa mbalimbali ya pembezoni mwa nchi hiyo ya  Kagera, Kigoma na Geita.
Jumanne jijini Dar es salaam Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dakta Emanuel Nchimbi ambaye wizara yake inahusika na idara ya uhamiaji ametoa taarifa ya zoezi la kuwaondoa wahamiaji haramu katika mkutano na waandishi wa habari.

Waziri Nchimbi kwanza alitoa ufafanuzi wa wahamiaji hao haramu ili kuondoa mkanganyiko unaoenezwa kwamba Tanzania imeamua kufukuza raia wa mataifa jirani.

Alisema wanaotakiwa kuondoka ni wale wanaoishi nchini kinyume na sheria ya uhamiaji inayowataka kuomba vibali maalum vya ukaazi na ufanyaji kazi hapa nchini

Kuna madai pia kwamba wahamiaji haramu walioamua kuondoka kwa hiari yao baada ya agizo la mkuu wa nchi Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, hawatendewi haki wengi wanaporwa mali zao na kufanyiwa uhuni.

Waziri wa mambo ya ndani amesema kufanya hivyo ni kosa kisheria na ndiyo sababu wametoa agizo la wahamiaji wanaotaka kuondoka na mali zao watoe taarifa kwa vyombo vya usalama ili polisi wawasindikize mpaka mpakani.

Wahamiaji haramu 10,672 wameshaondoka nchini Tanzania kuanzia kutangazwa kwa operesheni hiyo na Rais mwishoni mwa mwezi julai mwaka huu.
Ripoti ya Dina Chahali


Wahamiaji haramu waliorejea makwao kutoka nchini Tanzania  ni kutoka mataifa ya Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Tatizo la Wahamiaji haramu limekuwa kubwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Serikali imeahidi kuendesha operesheni ya kushtukiza wakati wowote kuanzia sasa kwa ajili  ya  kuwarejesha kwa nguvu wahamiaji haramu wote waliopo kwenye maeneo mbalimbali nchini


Share: