HIVI NDIVYO UFOO SALO ALIVYOJIOKOA

Baada tu ya kupata nafuu Mwandishi wa habari wa kituo cha ITV na Redio One asimulia baada ya kupata nafuu kutokana na kupigwa risasi hivi karibuni.Ufoo asimulia kama ifuatavyo

“Nyumbani kwetu, pale Kibamba si mbali sana na barabarani, wakati nikikaribia kufika barabarani wakati huo nikitokwa na damu nyingi huku nikihisi tumbo langu limejaa sana nilikutana na dada mmoja ambaye nilimuomba khanga ili nijifunge kuzuia damu zisitoke kwa wingi”.

Anasema dada yule alimpa khanga akajifunga na aliposogea barabarani alikutana na gari lililokuwa likiendeshwa na mwanamke mmoja.

“Nilipoona kuna gari linapita nikainuka kuomba msaada. Liliposimama nilimuona mwanamke akiendesha nikamweleza kwamba nilikuwa nimepigwa risasi na nilikuwa nikiomba msaada wake anikimbize hadi katika hospitali ya Tumbi na kwamba akifika pale tu aniache mlangoni.

“Si rahisi kuamini, yule mama alikataa kunisaidia akisema alikuwa akiwahi sehemu kumchukua mzazi. Sina la kusema niliamua kumsamehe tu yule mama ingawa niliumia sana,” alisema Ufoo.

Alisema muda mfupi tu baadaye alitokea kijana aliyekuwa na pikipiki, maarufu kwa jina la bodaboda ambaye alimuomba msaada wa kumkimbiza hospitali ya Tumbi na akakubali.

“Yule kijana aliniuliza iwapo nilikuwa ninao uwezo wa kujishikilia vizuri na niliposema nitaweza akanisaidia kupanda katika bodaboda.

“Wakati huo nilikuwa naona kama tumbo linazidi kujaa. Nikiwa kwenye pikipiki kuna wakati nilikuwa nikihisi kwamba naweza nikaishiwa nguvu na kuanguka katika barabara na kisha kupitiwa na gari na kupoteza maisha. Lakini nilipata ujasiri na kujishikilia,” alieleza kwa sauti ya chini
Share: