MASHIRIKA,WANAFUNZI WAPINGA ZIARA YA OBAMA AFRIKA KUSINI

Huku Rais Barack Obama wa Marekani akiwa amewasili nchini Senegal hii leo katika duru yake ya kwanza ya safari barani Afrika, safari yake hiyo inakabiliwa na upinzani mkubwa huko Afrika Kusini ambayo itakuwa nchi ya pili kuitembelea kabla ya kuelekea Tanzania.
Duru zinaarifu kuwa idadi kubwa ya mashirika ya wafanyakazi, wanafunzi wa vyuo vikuu, mawakili na watetezi wa haki za binaadamu wanapinga vikali safari ya Rais Obama nchini humo. Muungano wa Jumuiya za Wafanya Kazi Afrika Kusini COSATU umewataka wafanyakazi nchini humo kufanya maandamano ya kupinga safari hiyo. Katibu wa masuala ya kimataifa wa COSATU, Bongani Masuku amesema kuwa, siasa za Marekani zimejikita zaidi katika kuzalisha na kukithirisha silaha za nyuklia na kusambaza silaha ulimwenguni, jambo ambalo linavuruga amani, uadilifu, demokrasia na haki za binadamu.
Jumuiya ya Mawakili wa Kiislamu nchini Afrika Kusini imetaka Rais Barack Obama wa Marekani atiwe mbaroni kwa kutenda jinai za kivita. Jumuiya hiyo ya mawakili imetaka Obama afikishwe kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, (ICC) huko, The Hague, Uholanzi. Makundi ya kisiasa nchini Afrika Kusini yameitaja Marekani kuwa mporaji wa maliasili na utajiri wa nchi za Kiafrika.


Popular posts from this blog